Utangulizi
Ugonjwa wa Newcastle ni mojawapo ya magonjwa hatari zaidi yanayowasumbua wafugaji wa kuku duniani.
Ugonjwa huu unaweza kusababisha vifo vya kuku wengi ndani ya muda mfupi na kuleta hasara kubwa kwa wafugaji wa kuku wote na ndugu wote wafugwao.
Kwa bahati mbaya, wafugaji wengi hutambua ugonjwa huu ukiwa tayari umeenea kwenye banda. Ndiyo maana ni muhimu kufahamu dalili zake mapema na kuchukua hatua za kuzuia kabla haujasababisha madhara makubwa.
Ugonjwa wa Newcastle ni Nini?
Newcastle ni ugonjwa unaosababishwa na virusi (Newcastle Disease Virus – NDV). Virusi hivi hushambulia mfumo wa upumuaji, mfumo wa fahamu na mfumo wa mmeng’enyo wa chakula wa kuku.
Ugonjwa huu huambukiza kwa kasi sana na unaweza kuenea kutoka kwa kuku mmoja kwenda kwa wengine kupitia:
• Mate na makamasi ya kuku.
• Kinyesi cha kuku.
• Maji na chakula kilichochafuliwa.
• Viatu, nguo na vifaa vinavyoingia bandani.
• Ndege wa porini wanaoweza kubeba virusi.
Dalili za Ugonjwa wa Newcastlea
Dalili hutegemea aina ya virusi na umri wa kuku, lakini mara nyingi huonekana kama:
1. Kupumua kwa Shida
Kuku huanza kupumua kwa shida na kutoa sauti zisizo za kawaida.
Unaweza kuona:
• Kupumua kwa mdomo wazi.
• Kukohoa.
• Kupiga chafya.
• Kutokwa na makamasi puani.
2. Kukosa Hamu ya Kula
Kuku hupunguza ulaji wa chakula na maji.
Hii husababisha:
• Kudhoofika.
• Kupungua uzito.
• Ukuaji hafifu kwa Broiler
3. Kuharisha
Kuku wengi hupata kinyesi cha kijani cha kuharisha.
Hii ni dalili inayojitokeza mara nyingi wakati ugonjwa umeanza kuenea.
4. Kulegea na Kukaa Sehemu Moja
Kuku huonekana:
• Wamelala muda mwingi.
• Hawatembei sana.
• Mabawa yameshuka.
• Hawana nguvu
5. Dalili za Mfumo wa Fahamu
Hizi ndizo dalili zinazotisha zaidi.
Kuku wanaweza:
• Kupinda shingo.
• Kuzunguka bila mwelekeo.
• Kushindwa kutembea vizuri.
• Kupooza miguu au mabawa.
Dalili hizi huonyesha ugonjwa umefikia hatua mbaya.
6. Kushuka kwa Uzalishaji wa Mayai
Kwa kuku wa mayai unaweza kuona:
• Kupungua kwa idadi ya mayai.
• Mayai kuwa na gamba laini.
• Mayai kuwa madogo au yasiyo ya kawaida.
7. Vifo vya Ghafla
Katika baadhi ya aina za Newcastle, kuku wanaweza kufa ghafla bila kuonyesha dalili nyingi.
Hii ndiyo sababu ugonjwa huu huleta hasara kubwa kwa wafugaji.
Jinsi ya Kuzuia Newcastle
Kwa kuwa Newcastle husababishwa na virusi, kinga ndiyo njia bora zaidi kuliko kusubiri ugonjwa utokee.
1. Fuata Ratiba ya Chanjo
Chanjo ndiyo ulinzi mkubwa dhidi ya Newcastle.
Kwa kawaida:
• Siku ya 7 – Newcastle B1
• Siku ya 21 – Newcastle Lasota (Booster)
Usikose tarehe za chanjo.
Au unaweza fuata utaratibu huu kwa sehemu ambazo Gumboro ilishawahi kutokea
• Siku ya 14- Newcastle 1
• Siku ya 28-Newcastle Lasota (Booster)
• Rudia kila baadha ya miezi 3 kwa kuku wanaokaa bandani mda mrefu.
2. Imarisha Biosecurity
Zuia maambukizi kwa:
• Kudhibiti wageni wanaoingia bandani.
• Kusafisha banda mara kwa mara.
• Kutumia dawa za kuua vijidudu.
• Kutenga kuku wagonjwa.
3. Wape Lishe Bora
Kuku wenye lishe bora hujenga kinga nzuri zaidi.
Hakikisha chakula kina:
• Protein ya kutosha.
• Vitamins.
• Madini muhimu.
• Maji safi muda wote.
4. Epuka Msongamano
Msongamano mkubwa huongeza kasi ya maambukizi.
Fuata idadi inayoshauriwa kulingana na ukubwa wa banda.
5. Nunua Vifaranga Kutoka Sehemu Zinazoaminika
Anza na vifaranga vyenye afya kutoka kwa wasambazaji wanaoaminika ili kupunguza hatari ya kuingiza magonjwa shambani.
Je, Newcastle Inatibika?
Hakuna dawa inayoua virusi vya Newcastle moja kwa moja.
Matibabu yanayotolewa mara nyingi hulenga kusaidia kuku kupambana na madhara ya ugonjwa na kuzuia maambukizi ya bakteria yanayoweza kujitokeza baada ya kinga kushuka.
Hivyo, chanjo na biosecurity ndizo njia bora zaidi za kuzuia hasara.
Makosa Yanayofanywa na Wafugaji
• Kuruka ratiba ya chanjo.
• Kuhifadhi chanjo vibaya.
• Kutumia maji yenye chlorine au kemikali kuchabganyia chanjo
• Kununua vifaranga kutoka sehemu zisizoaminika.
• Kuruhusu wageni kuingia bandani bila tahadhari.
• Kutowatenga kuku wanaoonyesha dalili za ugonjwa.
Makosa haya yanaweza kuongeza hatari ya mlipuko wa Newcastle.
Hitimisho
Newcastle ni ugonjwa unaoweza kusababisha hasara kubwa kwa mfugaji ikiwa hautazuiwa mapema. Kutambua dalili zake kwa wakati, kufuata ratiba ya chanjo, kuimarisha biosecurity na kuhakikisha kuku wanapata lishe bora ni hatua muhimu za kulinda afya ya banda lako.
Kumbuka: Afya ya kuku wako ndiyo msingi wa mafanikio ya mradi wako wa ufugaji.
Amsterdam Group – Mshirika Wako wa Ufugaji
Amsterdam Group inatoa huduma na bidhaa mbalimbali kwa wafugaji, ikiwemo:
• Chanjo za kuku.
• Ushauri wa kitaalamu wa ufugaji.
• Vifaranga vya ubora.
• VITAMIX PLUS na virutubisho vingine.
• Premixes na Feed Additives.
• Vifaa vya kisasa vya ufugaji
Wasiliana nasi leo ili kupata ushauri na suluhisho bora kwa afya ya kuku wako.


